Serikali, Zitto ngoma nzito kuhusu CAG
Dar es Salaam. Wakati Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe akijiandaa kukata rufaa kupinga sehemu ya hukumu ya kesi ya kikatiba ya utumishi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), Serikali imemtangulia na kuweka kusudio la kukata rufaa.
Mahakama Kuu katika hukumu yake ya Desemba 5, mwaka huu chini ya majaji watatu, Dk Benhajj Masoud (kiongozi wa jopo) Juliana Masabo na Edwini Kakolaki, ilibatilisha uamuzi wa kuondolewa kwa Profesa Assad katika wadhifa huo kabla ya umri wake wa kustaafu ikisema hatua hiyo ilikuwa kuvunja Katiba.
Mahakama hiyo ilifikia uamuzi huo kufuatia kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na Zitto akipinga kifungu kifungu hicho cha 6(1) cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma Namba 11 ya mwaka 2008 kilichotumika kumuondoa Profesa Assad katika wadhifa huo.
Ingawa Mahakama ilikubaliana na Zitto kuwa kufungu hicho ni batili kwa kuwa kinakinzana na Katiba na kuwa Profesa Assad aliondolewa kinyume cha Katiba, ilikataa maombi ya kubatilisha uteuzi wa CAG wa sasa, Charles Kichere.
Kabla Zitto hajachukua hatua hiyo, Serikali imewasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa.
Taarifa hiyo ya kusudio la Serikali kukata rufaa ilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii na baadaye kuthibitishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk Eliezer Feleshi.
“Ninaitambua hii,” alisema Dk Feleshi kwa ufupi baada ya kuangalia nyaraka hiyo.
Baada ya kuwasilisha taarifa hiyo sasa Serikali inasubiri kupata kumbukumbu za shauri hilo kwa ajili ya kuwasilisha sababu za rufaa hiyo.
Mambo yakiwa hivyo upande wa Serikali, mmoja wa mawakili waliomwakilisha Zitto katika kesi hiyo, Dk Lugemeleza Nshalla alilieleza Mwananchi kuwa bado hawajawasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa na kwamba bado wanataka kukutana na mteja wao kuweka mambo sawa.
Profesa Assad aliteuliwa kushika wadhifa huo Novemba 5, 2014 na alihudumu katika nafasi hiyo kwa miaka mitano hadi Novemba 4, 2019, baada ya aliyekuwa Rais, Hayati John Magufuli kumteua Kichere kushika wadhifa huo kabla Profesa Assad hajatimiza muda wake wa utumishi kikatiba, yaani umri wa kustaafu.
Kufuatia hatua hiyo, Zitto aliiomba mahakama itamke kuwa kifungu hicho cha 6(1) cha Sheria ya Ukaguzi, ni batili kwa kuwa kinakinzana na Katiba na kwamba kuondolewa kwa Profesa Assad kabla ya kutimiza umri wa kustaafu ni batili na pia uteuzi wa Kicheria kuwa CAG mpya ilikuwa batili.
Alikuwa akidai kuwa Ibara ya 144(1) ya Katiba ambayo inaeleza kuwa CAG atatumikia wadhifa huo mpaka umri wake wa kustaafu, yaani miaka 60 kikatiba au 65 kwa mujibu wa kifungu 62(a) cha sheria hiyo ilikiukwa.
Wadaiwa katika kesi hiyo namba 8 ya mwaka 2020 walikuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Kichere na Profesa Assad.
Mahakama hiyo katika hukumu yake ilikubaliana na hoja za Zitto kuwa kifungu hicho cha 6(1) cha Sheria ya Ukaguzi kuweka mihula ya miaka mitano mitano ya utumishi wa CAG ni batili kwa kuwa kinakinzana na Ibara ya 144 ya Katiba.
Mahakama ilisema wakati kifungu hicho kinaweka mihula ya utumishi wa CAG, Katiba inazungumzia umri wa kustaafu na si mihula.
Hivyo ilisema kuwa kuondolewa kwa Profesa Assad kabla ya kufikisha umri wa kustaafu kulikuwa ni batili, hata hivyo ilikataa maombi ya Zitto kutaka uteuzi wa Kichere utangazwe ni batili, badala yake imesema uteuzi wake ni halali kwa kuwa aliteuliwa kwa mujibu wa Katiba na anazo sifa za kuwa CAG.
Maoni
Chapisha Maoni