Sababu picha ya Rais, bendera kupandishwa Dubai hii hapa
WEDNESDAY MARCH 02 2022
Juzi, ilisambaa video kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha bendera ya Tanzania ikiwa imefunika jengo hilo refu duniani lililopo Dubai.
Leo Jumatano Machi 2, 2022 Dk Kijaji wakati akizungumzia mafanikio ya ziara ya Rais Samia aliyoifanya katika nchi za Ufaransa, Ubelgiji na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) amezungumzia suala hilo akisema hiyo ni moja ya mafanikio ya ziara hiyo.
Amesema kuwa bendera hiyo ambayo ilipandishwa kwenye jengo refu kuliko yote duniani ilipandishwa usiku wa kuamkia Jumanne ikiwa ni kuitangaza Tanzania na fursa zinazopatikana.
“Wote tumeona kilichotokea kule Jiji la Dubai, kuonyesha umuhimu wa ziara ya Rais aliyoifanya, ndani ya Jiji la Dubai walionyesha bendera ya Tanzania kwenye jengo kubwa zaidi duniani kama zawadi kwa Rais na Taifa letu’ amesema Dk Kijaji
Amesema kuwa siku moja baada ya kupandishwa bendera hiyo, usiku uliofuatia ilipandishwa tena pamoja na picha ya Rais Samia
“Jana te bendera ya Taifa letu ikiwa na picha ya Rais wetu hasa tukiwa kwenye mwezi huu wa tatu ambao tunasherekea malkia wa nguvu pote duniani na Tanzania tukiongozwa na malkia wa nguvu mama yetu Samia” amesema
Amesema kuwa hiyo moja ya njia ya kuonyesha na kutangaza fursa zinazopatikana Tanzania na kuwataka Watanzania kutarajia kuendelea kuona fursa zikiendelea kutangazwa kwenye jengo hilo.
“Katika kuendelea kuitangaza na kuuza fursa tulizonazo, Watanzania watarajie siku ya leo wataona pia bendera yetu ikiendelea kupandishwa kwenye jengo lilelile na leo hii tutakuwa na picha ya Mlima Kilimanjaro” amesema
Amesema hizo ni jitihada za kuitangaza Tanzania kwa wawekezaji kuwa nchi iko salama na ina fursa nyingi za uwekezaji na itafanyika kwa mwezi mzima.
Maoni
Chapisha Maoni