Kajala Kupelekwa Mahakamani Baada ya Kumtosa Harmonize Kudaiwa Fidia Kwa Makosa Mawili
MADAI yanayoendelea mitandaoni kuwa penzi la mwigizaji Kajala Masanja na msanii Rajab Kahali ‘Harmonize limevunjika limekaa vibaya kisheria.
Endapo jambo hili ni kweli, Kajala anakabiliwa na hatari ya kupelekwa mahakamani kufunguliwa mashtaka kwa makosa mawili.
Kifungu cha 69( 1 ) cha Sheria ya Ndoa iliyofanyiwa marekebisho 2010 kinasema kuwa mtu anaweza kufungua shauri na kudai fidia baada ya uchumba kuvunjwa.
Ifahamike kuwa katika siku za hivi karibuni Kajala na Harmonize walijitangaza kuwa ni wachumba baada ya mwanaume huyo kumvisha pete mwanadada huyo, jambo ambalo linawaweka wawili hao katika hatari ya kufikishana kortini kidaiana fidia na zawadi.
Kudai fidia na kurudisha zawadi ni vitu viwili tofauti ambavyo vyote vinaweza kumtia mmoja wa wachumba kwenye kasheshe ya kisheria.
Kwa tafsiri rahisi fidia inahusu kulipwa maumivu aliyopata mmoja wa wachumba (mume au mke) kutokana na tukio hilo la kuachwa pamoja na muda aliopotezewa na aliyekuwa mchumba wake.Aidha, zawadi ni mchumba kuiomba mahakama imuamuru mtuhumiwa arejeshewe mali zote alizotoa mlalamika wakati akiyaishi maisha ya uchumba na mwenzake.
Masharti ya kufungua shauri kwa mujibu wa sheria na kifungu tajwa ni kuwa , MOJA anayefungua shauri awe ni yule aliyeumizwa.
PILI; ahadi ya kuoana lazima iwe ilikuwa imefanyika ndani ya mipaka ya Tanzania na TATU; wakati mnaingia kwenye uhusiano wote muwe mlikuwa mmetimiza miaka 18 au zaidi.
Kifungu cha 71 cha Sheria ya ndoa ya mwaka 1977 kinasema kuwa mtu anayo haki ya kufungua shauri kudai kurejeshewa zawadi ambazo alizitoa kwa mtu ambaye alikuwa ana ahadi ya kufunga naye ndoa lakini ndoa haikufungwa.
Zawadi zinaweza kuwa ni pamoja na fedha, nyumba, magari, nguo na kila kitu chenye thamani (valuable).
Msisitizo ni kwamba, haijalishi mali hiyo ipo kwenye jina la nani suala la msingi ni kuthibitisha kuwa mlalamikaji ndiye uliyetoa hiyo zawadi.
Ni wapi mlalamikaji anaweza kufungua shauri hilo? Sheria inaweka wazi kuwa ni; mahakama yoyote ya mwanzo, ya wilaya, ya hakimu mkazi au hata mahakama kuu.
Hata hivyo, uamuzi wa wapi sehemu sahihi pa kufungulia madai itategemea na thamani ya kiwango cha mali kinachodaiwa.
Ingawa sheria inawapa haki wachumba wote wawili kuchukua hatua ya madai kwa hili la Harmonize na Kajala, mwanamke huyo yuko hatarini zaidi kutokana na kuwepo kwa taarifa nyingi za kupatiwa zawadi mbalimbali yakiwemo magari ya kifahari na mchumba mchumba wake.
Kwa msingi huo, kama Kajala atathibitika kupewa zawadi hizo mbele ya mahakama atalazimika “azitapike” zote bila kujali kama ameshazitumia, kuzigawa au kuziuza.
Sheria inasema kama mali hizo zitakuwa zimekwishatumika au hazipo tena mlalamikiwa atatakiwa kulipa fedha zinazolingana na mali hizo au kuzinunua nyingine mpya.
Inaelezwa kuwa, endapo mlalamikiwa atashindwa kurudisha mali alizopewa kama zawadi ya uchumba basi mali zake binafsi ambazo hazikuwa sehemu ya zawadi zitauzwa ili kupata kiwango kinachodaiwa na likishindikana hilo mlalamikiwa atatakiwa kwenda jela kama mfungwa wa madai.
Sheria hii ya ndoa imelifanya jambo la uchumba kuwa kitu cha kuheshimiwa tofauti na baadhi ya watu wanaodhani ni suala la mchezomchezo kiasi cha kuchumbiana na kuachana kiholela.
Maoni
Chapisha Maoni