Mzozo wa Ukraine: Fahamu kwanini baadhi ya mataifa yenye uwezo mkubwa yamesalia kimya
Mzozo wa Ukraine unaoendelea ukikaribia wiki moja sasa umeigubika siasa ya dunia. Wakati sehemu kubwa ya dunia ikionesha mshikamano na taifa hilo dhidi ya uvamizi wa jirani yake mkubwa, Urusi na mataifa mengi kuilaani Urusi, wanachojiuliza walimwengu ni kwa nini nchi nyingine zimekaa kimya Urusi na kiongozi wake Vladimir Putin wakiwekewa vikwazo vikali?.
Nini kiko nyuma ya uamuzi wa kubakia kimya kwa nchi zenye nguvu kisiasa na kiuchumi katika kanda zao na duniani, kama vile Iran, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, India, China na Korea Kaskazini?
Mchambuzi wa makala hii ana mtazamo ufuatao.
Saudi Arabia na UAE
Saudi Arabia na Urusi zinatajwa kama nchi mbili zenye nguvu zinazochimba mafuta na kwa pamoja zinatoa karibu robo ya mafuta yasiyosafishwa (ghafi) duniani. Saudi Arabia pia ni nguvu kubwa ya kiuchumi katika Ulimwengu mzima wa Kiarabu. Hapa ni masilahi ya kiuchumi yenye nguvu.
Pamoja na Saudi Arabia kuwa mwanachama wa Jumuiya ya nchi zinazosafirisha mafuta kwa wingi duniani (OPEC) lakini Mwanamfalme na mrithi mteule wa kiti cha Ufalme, Mohammed bin Salman amekuwa akisisitiza juu ya nchi yake kuheshimu makubaliano na Urusi kuhusu suala la mafuta.
Hili limeonekana hata wakati Urusi ilipoanza kujiandaa kwa uvamizi wa Ukraine. Lengo la Saudi Arabia ni kutuliza msukosuko wa bei ya mafuta katika soko la dunia. Tayari siku chache tu baada ya uvamizi wa Urusi, bei ya mafuta ghafi ilipanda hadi dola 100 kwa pipa.
Falme nyingine ya Kiarabu katika eneo la Ghuba, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) imejizuia kuwa upande wowote ikisema inataka kushajiisha suluhisho la kisiasa katika mgogoro wa Ukraine na Urusi, kwani kuunga mkono upande mmoja wapo ni kupalilia machafuko.
Bila shaka UAE ina wasiwasi na vikwazo vilivyotangazwa na Marekani, Umoja wa kujihami wa nchi za magharibi (NATO), Umoja wa Ulaya na nchi nyingine dhidi ya Urusi, kwa sababu kampuni zake kubwa zimewekeza mabilioni ya dola katika uchumi wa Urusi, mbali na mikataba minono ya ununuzi wa zana za kijeshi kutoka Urusi.
Uhusiano wa Iran na Urusi
Kutokana na hatua ya mataifa ya magharibi kuiwekea Iran vikwazo vya kiuchumi, kutokana na mpango wake wa Kinyuklia ambao Iran inadai ni kwa ajili ya nishati, taifa hilo limegeuka mshirika mkubwa wa kibiashara wa Urusi na hasa panapohusika na akiba ya mafuta na akiba kubwa ya mafuta ya taifa hilo la Uajemi.
Katika safu ya kisiasa na kijeshi, mataifa haya mawili yamekuwa washirika katika mizozo kuanzia Syria na Iraq. Vilevile washirika wakati wa mzozo wa Afghanistan. Iran ina ushawishi mkubwa pia katika nchi za Asia ya Kati zilizokuwa zamani sehemu ya Muungano wa Kisovieti wa Jamhuri 15. Muungano huo ulisambaratika 1989 kufuatia kuporomoka kwa ukoministi.
Kwa upande wa India, inaonekana kuweka masilahi yake ya kitaifa kwanza na hivyo msimamo wake wa kujizuia kuilaani Urusi juu ya uvamizi wake wa Ukraine haukushangaza. India inashirikiana kwa kiwango kikubwa na Urusi katika sekta ya kijeshi na teknolojia na mwezi Machi mwaka huu zilisaini mkataba mpya wa miaka 10 wa ushirikiano katika sekta ya ulinzi.
Inaposimama India
India inaiegemea Urusi ikimuangalia jirani yake China kuwa ni kitisho. Kwa muda mrefu dola hizi mbili kubwa barani Asia zimekuwa na uhasama na mvutano wa mpaka wa eneo la kaskazini mwa China la mlima wa Himalaya. Kufuatia mgogoro huo, mwaka 2020 zilipigana vita vikali.
Kuna suala la mvutano na jirani yake Pakistan ambayo kabla ya kuundwa kwake 1947 baada ya uhuru kutoka kwa Uingereza ilikuwa sehemu ya India iliyo kubwa. Wakati India imekuwa sahiba wa Urusi tokea enzi ya Muungano wa Kisovieti, nayo Pakistan ina usuhuba mkubwa na China.
Sababu moja kubwa ya India kujizuia kulaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine wakati wa mjadala kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ni mgogo wa Kashmir, eneo linalokaliwa na India.
Kwa miaka mingi inavutana na Pakistan kuhusu eneo hilo ambalo Pakistan inadai ni sehemu yake na kuitaka India iwape fursa wakazi wa Kashmir kuamua kama wanataka kubakia sehemu ya India au kujiunga na Pakistan. Uhasama wao ulisababisha vita 1965 na baadaye tena India kusaidia kumeguka kwa eneo la mashariki mwa Pakistan baada ya vita vya 1971 na kuundwa Bangladesh.
Karata ya diplomasia ya China
China upande wake imekuwa ikicheza karata ya diplomasia ya kuuma na kupuliza kwa pande zote mbili Ukraine na Urusi. Lakini wakati ikitoa wito wa suluhisho la amani ni wazi imeshindwa kwenda mbali zaidi kulaani uvamizi wa Urusi kwa sababu nchi hizo mbili zilikuwa zote wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zenye kura ya turufu kwanza zinahitajiana katika masuala yayohusika na siasa za dunia.
Kubwa ikumbukwe China ingali ikidai Taiwan ni sehemu ya ardhi yake. Kwa hivyo kusita kuilaani Urusi ni mkakati wa kutafuta kuendelea kuungwa mkono na Dola hilo kubwa jirani. China ilihakikisha inaizuia mitandao nyumbani kutochapisha chochote kinacholaani uvamizi huo wa Urusi.
Kiuchumi China ina ushirikiano mkubwa na Urusi kuliko nchi nyingine yoyote. Uhusiano wa kibiashara ni kuanzia ununuzi wa mafuta, makaa ya mawe hadi nafaka na hasa ngano. Urusi ikiwa ni nchi ya kilimo ni muuzaji mkubwa wa ngano duniani. Urusi pia yenye mpaka wa maili karibu 2,700 ni soko kubwa la bidhaa kutoka China. Bidhaa hizo ni pamoja na za viwanda.
China imekuwa na uhusiano mzuri wa kibiashara na Ukraine na ndiyo maana katika kile kilichoonekana kuwa mgogoro huu ni wenye kuisumbua sana China, ikatoa wito wa uvumilivu na mazungumzo kuutatua, pamoja na kufahamu fika kwamba si jambo rahisi. Shabaha yake ni kutoathiri uhusiano wake na pande zote mbili
Maoni
Chapisha Maoni