Dodoma. Zimwi la mgogoro ndani ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT) limeendelea na kusababisha mkutano kuvunjika.
Leo Alhamisi Desemba 15, 2022, mkutano huo ulianza kwa mashaka kwani viongozi waliopewa nafasi ya kuzungumza walieleza namna CWT inavyokabiliwa na migogoro, mpasuko wa makundi.
Mara Baada ya kuhutubia, mgeni rasmi, Profesa Joyce Ndalichako kwa niaba ya Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, wajumbe walipumzika kwa ajili ya chakula lakini waliingia ukumbini saa 8:40 mchana huku viongozi wakiingia saa 10:39 jioni.
"Tulikuwa na majadiliano na msajili na viongozi wa Serikali kuhusu kilichotokea jana, tumekubaliana sasa msajili azungumze kisha Katibu wa Tucta na mkutano uahirishwe hadi kesho ili baraza likutane kwanza," amesema Kaimu Rais wa CWT, Dinah Mathamani.
Kauli hiyo ilizua mzozo na kelele nyingi kwa wajumbe ambapo walisimama na kuanza kuimba wimbo wa mshikamano huku wakidai posho zao.
Mwekahazina wa CWT, Rotas Magesa alisimama na kuwatangazia wajumbe kilichochelewesha posho hizo ni suala la mtandao wa benki lakini akawaahidi ndani ya saa moja posho hizo zingekuwa kwenye akaunti zao, akaomba wawe watulivu.
Mkutano wa CWT umevunjika kwa kilichoelezwa bado kuna maelekezo ya Serikali na Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi.
Mathaman ametangaza kuahirisha mkutano hadi kesho huku baraza la chama likitakiwa kukutana na Katibu wa Tucta na Msajili.
Wakati wanatoka ukumbini, wajumbe kulikuwa na kelele nyingi na makundi ambayo yalizungumzia kutokuwa na imani na viongozi wao kwa madai kwamba wanawapeleka vibaya.
Maoni
Chapisha Maoni