l
Chadema yatangaza kuanza mikutano ya hadhara
Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewataka waliokuwa wagombea ubunge katika uchaguzi mkuu 2020 kufanya maandalizi ya mikutano ya hadhara kwenye maeneo yao.
Hayo yameelezwa ikiwa ni mwezi mmoja tangu chama hicho kilipotangaza msimamo wa kuanza mikutano ya hadhara mwisho wa mwaka huu.
Novemba mwaka huu mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, John Heche akiwa wilayani Sengerema alisema ndani ya kipindi cha mwezi mmoja watatangaza ratiba na kuanza mikutano ya hadhara.
Akizungumza leo Jumatano Desemba 14, 2022 wakati akifungua semina ya siku mbili ya waliokuwa wagombea ubunge, Katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika amesema ni wajibu wa vyombo vya chama kuanza maandalizi ya mikutano hiyo.
"Septemba Kamati Kuu ya chama ilikaa na mojawapo ya kilichokubaliwa ni kuanza mikutano ya hadhara, kafanyeni maandalizi kwenye maeneo yenu na kutoa taarifa ili tuweze kuanza," amesema.
"Ni wajibu kwa vyombo vyote vya chama kuanzia ngazi ya Kanda na mabara kufanya maandalizi ili tujue lini tunaanza,"amesema Mnyika.
Mnyika amesema haki ya kujumuika ni haki mama kwa vyama vya siasa hivyo ni lazima hilo lisimamiwe.
"Tunaendelea kudai na ni lazima haki hii ipatikane, kwani ukitaka kuruka lazima uagane na nyonga," amesena.
Serikali ilizuia mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa mwaka 2016, ikitaka wananchi wajikite kwenye shughuli za maendeleo hadi wakati wa chaguzi nyingine.
Hata hivyo kikosi kazi cha kukusanya maoni ya demokrasia kilichokabidhi ripoti hiyo kwa Rais Samia Suluhu, Oktoba 21 mwaka huu, pamoja na mambo mengine kilipendekeza mikutano ya vyama vya siasa iruhusiwe.
Maoni
Chapisha Maoni