Wananchi Tanzania walalamika na kupinga viwango vya Bima ya afya
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Profesa Abel Makubi wakati wa kikao na wakurugenzi wa wizara na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya Tanzania.
Wananchi wameilalamikia Serikali ya Tanzania na kupinga hatua ya Wizara ya Afya kupendekeza viwango vya kulipia Bima ya afya ambavyo ni Sh. 340,000 kwa kaya ya watu 6 na Sh. 84,000 kwa mtu mmoja asiye na familia katika kipindi cha mwaka mmoja.
Kiwango hicho kinapigwa vita na wananchi walio wengi kutokana na hali ya ngumu ya maisha nchini humo.
Ingawaje kwa muda mrefu ni wananchi wachache nchini Tanzania ndiyo wenye uhakika wa matibabu kwa kuwa na bima ya afya huku asilimia 85 ya wengine wakikosa huduma hiyo.
Hata kulingana na takwimu hizi, Serikali imeshindwa kuwakomboa wananchi wake kwa kupendekeza viwango rafiki vitakavyopelekea kila mwananchi kuweza kulipia bima hiyo bila usumbufu wowote.
Zuberi Mkalaboko Mkazi wa Morogoro amesema viwango vilivyopendekezwa na Wizara havitawasaidia wananchi kumudu kulipa kutokana na hali duni ya kiuchumi na hivyo kuitaka Serikali kupendekeza viwango vinavyolingana na hali za raia wake.
Hata hivyo watanzania wengi waliposikia mipango ya Serikali ya kila Mtanzania kupata bima ya afya walifarijika lakini viwango vilivyowekwa vimeleta sintofahamu.
Hassan Shechambo Mkazi wa Kibaha picha ya Ndege amesema kama Serikali haitaweka viwango rafiki na kutoa elimu juu ya umuhimu wa bima ya afya wananchi wanaweza kukwepa matibabu hayo na kukimbilia katika miti shamba ili kukwepa gharama kubwa za viwango vya bima vilivyowekwa.
Salma Ramadhani Mkazi wa Kimara Dar es Salaam amesema kama dhamira ya Serikali ni kuwasaidia watanzania basi wana wajibu wa kupunguza walivyopendekeza namna ya kulipia huduma hiyo.
Shughuli nyingi za maendeleo zinaweza kukwama ikiwa wananchi wake afya zao si imara hivyo hakuna jambo lililo kubwa kama bima ya afya ya umma kwa wote.
Maoni
Chapisha Maoni