Waziri Makamba anateswa zaidi na siasa za nchi kuliko Tanesco
SATURDAY FEBRUARY 26 2022
Post-truth politics ni msamiati wa kisiasa wenye maana ya siasa zinazoongozwa kwa utamaduni wa kusema uongo mwingi na ukweli kidogo. Zama ambazo uongo hutawala zaidi kisiasa huitwa “post-truth era”.
Ni muundo wa siasa ambao uongo hutumika zaidi kuuhadaa umma. Utamaduni wa kuogopa ndio umekuwa ukitawala siasa za Afrika na maeneo mengi duniani. Ukweli ni mdogo kwenye majukwaa ya siasa.
Februari 15, mwaka huu, Waziri wa Nishati, January Makamba, alitoa ufafanuzi bungeni kuhusu hali ya mafuta kupanda bei, vilevile hali ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na tatizo la umeme na mambo mengine kwenye wizara yake.
Weka pembeni hoja zenye kubeba ukweli (facts), yapo mambo aliyagusia. Kwamba kulikuwa na mashambulizi binafsi ndani ya Bunge. Akasema, kama kuna tatizo yeye kuwa waziri au Samia Suluhu kuwa Rais, wazungumze kwa mambo mengine lakini sio mashambulizi binafsi.
Kwamba wakati Watanzania wakihitaji kuona tatizo la umeme linafika ukomo na majibu yanapatikana, katika siasa kuna minyukano ya kwa nini January awe waziri, au eti Samia kuwa rais.
Februari 2008, Edward Lowassa, alipokuwa anatangaza kujiuzulu uwaziri mkuu, alisema, kuingizwa kwake kwenye kashfa ya Richmond, tena bila kupewa haki ya kujitetea hakukuwa kwa bahati mbaya, akasema lilikuwepo tamanio ambalo alitakiwa kulitimiza. Nalo ni uwaziri mkuu. Akajiuzulu!
Yaani, Lowassa aliamini watu hawakupenda yeye kuwa waziri mkuu, ndio maana akaingizwa kwenye kashfa ya Richmond ili ionekane waziri mkuu alifanya madudu. Kwa hiyari yake, akatangaza kubwaga manyanga. Historia ikaandikwa.
Ni siasa za nchi. Ukweli unaweza kufanywa uongo, vilevile uongo kugeuzwa ndio ukweli na umma utaelezwa na kulazimishwa uamini. Au uongo unapakwa rangi ya kuvutia, unapendwa na unawekwa kwenye kabati la ukweli. Ya kweli yanapuuzwa, yanayoaminiwa na ya uongo yaliyonakshiwa rangi nzuri.
Mathalani, January katika maelezo yake bungeni, aligusa eneo la takwimu ya mapato ya nchi, Novemba 2020 dhidi ya Novemba 2021, kisha Desemba 2020 dhidi ya Desemba 2021. Hiyo ni kwa mujibu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
January alieleza kuwa mapato ya nchi Novemba 2020 yalikuwa Sh1.3 trilioni na Novemba 2021 yakawa Sh1.7 trilioni. Ongezeko la Sh400 bilioni. Vilevile Desemba 2020 mapato yalikuwa Sh2.0 trilioni, wakati Desemba 2021 TRA walikusanya Sh2.4 trilioni.
Hapo January alikuwa anajibu hoja kuhusu kwamba uchumi unaporomoka tangu Rais Samia aliposhika usukani. Akaelekeza wabunge kusoma ripoti za TRA ili waone ongezeko la mapato ya nchi chini ya Rais Samia. Akaeleza kuwa ukuaji huo wa mapato ni kwa sababu viwanda vinapata umeme na vinazalisha.
January alifafanua kwamba wakati mwingine viwanda havipti umeme na wananchi wanapata, kuna kipindi wananchi mtaani wanakosa na wenye viwanda wanapewa ili wazalishe. Akasema, ingewezekana kuwanyima umeme viwandani na kuwaambia wafunge midomo, halafu mtaani uwe mwingi.
Kauli hiyo ya January, “ingewezekana kuwanyima umeme viwandani na kuwaambia wafunge midomo, halafu mtaani uwe mwingi”, inaamsha maswali je, kuna wakati imewahi kutokea hivyo?
Viwanda vinakosa umeme na kunyamazishwa halafu mtaani umeme unakuwa wa kutosha ili ionekane hakuna tatizo kabisa?
Ukichukua maneno hayo ya January na kuyatafsiri kwa mtindo wa katikati ya mstari, hutakosea ukitafsiri kuwa zilikuwepo nyakati za viwanda kukosa umeme na kuambiwa wasiongee chochote. Mtaani kuonekane shwari kumbe hali si shwari. Hizo nyakati ndizo zinapaswa kuitwa post-truth era!
Tanesco na umeme
Mtindo wa siasa za nchi ni sababu ya January kuonekana kuteswa na hoja za wanasiasa wenzake kuliko matatizo ya umeme ambayo amekuwa akijinasibu kuyatatua. Kwamba aliyakuta na anayafanyia kazi.
Ni kama ambavyo Rais Samia mpaka leo analazimika kujifafanua ili aeleweke kwa wasioamini kama yeye ni rais mwenye mamlaka kamili.
Katika ufafanuzi wake bungeni, alieleza tatizo la Serikali kutorejesha asilimia 10 mpaka 12 za mapato ghafi ya Tanesco kwa ajili ya ukarabati na matengenezo. Serikali inatumia fedha zote kwenye matumizi mengine. Hivyo, Tanesco wamekuwa wakiendesha mitambo kwa miaka mingi bila ukarabati wala matengenezo ya uhakika.
Hilo la matengenezo na ukarabati, Tanesco, liliibuliwa pia na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Apili 2019, wakati huo ofisini akiwa Profesa Mussa Assad. Alieleza kuwa tatizo la kukatika umeme mara kwa mara lilisababishwa na ubovu wa mitambo iliyokosa matengenezo ya uhakika.
Angalau hapa tunakumbushana, kwamba tatizo la umeme lipo. Mwaka 2019, umeme kukatika mara kwa mara ilikuwa hoja ya CAG. Wakati huo, Rais alikuwa Dk John Magufuli na Waziri wa Nishati aliyekuwepo ofisini ni Medard Kalemani.
Dhambi ni kusema tatizo la umeme limeanza wakati wa Rais Samia au kipindi cha uwaziri wa January. Hoja ambayo tunaweza kujadili ni kwa nini January anazungumza masuala ambayo Kalemani hakuyatamka kabisa?
Mfano, January anaeleza changamoto ya ubovu wa mitambo, anafafanua uduni wa miundombinu. Anaujulisha umma kuwa Tanesco wamekuwa wakitumia nyaya za kusambazia umeme kusafirishia nishati hiyo.
Nyaya zinazotumika kusafirisha umeme ni zile zenye uwezo wa kubeba umeme wa msongo mkubwa, kuanzia kilovolt 400, 220, 132 na za chini kabisa ni kilovolt 66. Zinazosambaza umeme ni za msongo mdogo, kilovolt 33 na kilovolt 11. Kwa sasa, Tanesco wanasafirisha umeme kwa nyaya zenye uwezo wa kusambaza tu.
Yaani waya ambao unatosha kusambaza umeme ili ukufikie nyumbani kwako, ndio unaotumika kusafirisha kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine. Haya ni mambo ambayo hayakuwa yakizungumzwa kabla. Ni kwa sababu ya siasa au woga? Wahusika na Mungu wao, ndio wanaojua.
Inaelezwa, kuna uhaba wa transfoma. Uwezo wa transfoma moja ni kuhudumia nyumba 100. Kwa sasa, transfoma moja inahudumia nyumba mpaka 159 mpaka 180. Zinazidiwa, zinajizima. Suluhu ni kuongeza transfoma za kutosha.
Kwa nini ufafanuzi huu unakuja kipindi cha January? Huko nyuma matatizo hayakuwepo? January anasema ameyakuta na anayashughulikia. Na anaomba kupimwa kwa matokeo.
Kipindi cha Kalemani, nchi ilishuhudia maagizo ya saa na siku ili mgao wa umeme usiwepo. Maagizo yalitatua matatizo au yaliahirisha kwa muda? CAG Assad alisema Aprili 2019 kuwa hali ya Tanesco ni mbaya na January anasema amekuta matatizo mengi.
Kwa mwenye kupenda matokeo chanya, angependa aelezwe hali halisi. Na daktari anayeuelezea vizuri ugonjwa wa mtu, ni rahisi kuutibu. Hapa namwona January. Hata hivyo, yupo ambaye haamini sayansi, atasema mgonjwa haumwi ila karogwa. Huo ni ushirikina.
Wataalamu wenye eneo lao wakieleza tatizo la Tanesco ni uchakavu wa mitambo na uduni wa miundombinu, wewe ukisema wataalamu wanaliroga shirika, huo ni ushirikina. Inaonekana January anajaribu kujitenga na ushirikina.
Kuna ripoti mpya kuwa kiwango cha matumizi ya umeme kwa siku kimepanda mno. Hiyo ni kwa sababu ya ongezeko la shughuli za kiuchumi. Shirika ambalo limekuwa likitajwa kuwa ni dhoofu’lhali miaka nenda rudi, linaweza kweli kumudu kasi ya sasa ya ukuaji wa shughuli za uchumi?
Turuhusu ukweli uongoze siasa za nchi. Uongo usiongoze ukweli. Kama January alivyofafanua kwa kueleza ndivyo ilivyo kitaalamu, mwingine aje na hoja za kitaalamu kupinga. Vinginevyo, utaalamu ukidhibitiwa na siasa ni ushirikina. Nchi haiwezi kuongozwa kishirikina. Tanesco haitakombolewa kwa ushirikina
Maoni
Chapisha Maoni