Viongozi wa dini wamwomba Rais Samia kumaliza kesi ya Mbowe
WEDNESDAY MARCH 02 2022
Dar es Salaam. Wakati Mwenyekiti wa Chadema na wenzake watatu wakianza kujitetea Ijumaa Machi 4, 2022 katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, viongozi wa dini wamemwomba Rais Samia Suluhu Hassan kutumia busara kumaliza kesi hiyo.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Zuhura Yunus kwa vyyombo vya habari leo Jumatano imesema viongozi hao walikutana na Rais Samia Ikulu ya Dar es Salaam, ambapo pamoja na mambo mengine wamejadili masuala ya maendeleo ya nchi.
“Viongozi wa dini wametumia mkutano wao na Mhe. Rais Samia kuomba mamlaka husika kutumia busara ili kuangalia namna ya kumaliza kesi inayomkabili kiongozi wa Chama cha cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake,” imesema taarifa hiyo.
Mbali na suala hilo taarifa hiyo imesema viongozi hao pia wamejadili elimu, ambapo wamependekeza kuwepo na mjadala mpaka kuhusu mfumo mpya utakaokidhi mahitaji ya sasa kwa maana kutozalisha jamii ya wahitimu walioandaliwa kuajiriwa peke yake.
“Vilevile wameomba kutotozwa kodi ya mapato kwenye fedha ambazo zinapatikana kama misaada ya hiari ya wanachama na wafadhili kwa ajili ya kuendesha huduma zisizo za kibiashara zikiwemo huduma za wajane na yatima.
“Suala la uchafuzi wa mazingira nalo limepewa kipaumbele huku viongozi hao wakitoa wito kwa Serikali kuhamasisha upandaji wa miti ya asili badala ya miti na mbegu kutoka nje ambazo nazo zinahatarisha usalama na afya za wananchi,” imesema taarifa hiyo.
Maoni
Chapisha Maoni