Majeshi ya Russia yamuua mwanachuo wa India akiwa dukani
WEDNESDAY MARCH 02 2022
Raia wa India, Naveen Shekharappa Gyanagoudar, aliyeuawa wakati jiji la Kharkiv likishambuliwa jana (Jumanne), alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Chuo Kikuu cha Afya cha Kharkiv, Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Harsh Shringla amesema jana katika kikao na waandishi.
“Alikuwa ametoka nje kununua mahitaji na kubadili fedha wakati alipouawa,” binamu yake Kantesh Gyanagoudar amesema akizungumza na CNN leo (Jumatano).
Amesema Naveen alikuwa amepanga kuondoka kwenda Poland mapema zaidi ya siku hiyo.
Shringla amesema Naveen alikuwa akisubiri kununua mahitaji katika duka wakati alipopigwa na bomu.
Naveen alikuwa amezungumza na baba yake muda mfupi kabla ya kwenda nje kufanya manunuzi, na pia alizungumza na mama yake mapema Jumanne, amesema Kantesh.
Hadi Jumanne jioni, mwili wake ulikuwa katika chumba cha kuhifadhia maiti chuoni kwake, amesema Shringla, akiongeza kuwa maofisa wa India wako kwenye mawasiliano na wenzao wa jiji hilo kwa ajili ya kuusafirisha mwili.
“Tunaomba serikali ya India iurejeshe nyumbani mwili wake mapema iwezekanavyo. Na iwarejeshe nyumbani wanafunzi wote wa India. Hatutaki tukio kama hili lijirudie,” amesema Kantesh.
Waziri Mkuu wa India, alituma salamu za kueleza alivyoguswa na kifo hicho.
Shringla amesema ameongea na mabalozi wa Russia na Ukraine kusisitiza usalama kwa raia wote wa India ambao bado wako Kharkiv na katika miji mingine yenye vita.
Maoni
Chapisha Maoni