Guterres na Shahid wazungumza baada ya azimio kupitishwa
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limezungumza na kama Katibu Mkuu ni wajibu wangu kusimamia azimio hili na niongozwe na wito wake,” amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wakati akizungumza na waandishi wa habari punde tu baada ya Baraza hilo kupitisha azimio kuhusu uvamizi wa Ukraine uliofanywa na Urusi.
Azimio hilo limepigiwa kura ambapo nchi wanachama 141 wa Umoja wa Mataifa wameliunga mkono huku 5 zikipinga na 35 hazikuonesha msimamo wowote.
Katibu Mkuu amesema “ujumbe wa Baraza Kuu ni thabiti na dhahiri. Maliza chuki nchini Ukraine sasa! Sitisha mashambulizi sasa! Fungua milango ya mazungumzo na diplomasia sasa! Mamlaka ya kieneo na uhuru wa Ukraine lazima viheshimiwe kwa mujibu wa Chata ya Umoja wa Mataifa.”
Guterres amesema hivi sasa hakuna muda wa kupoteza.
Jumla ya nchi 96 wanachama wa Umoja wa Mataifa zilishiriki katika uwasilishaji wa azimio hilo ambalo lilihitaji theluthi mbili tu ya kura za ndio ili liweze kupita.
Kwa upande wake Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Abdullah Shahid amewaeleza waandishi wa habari kuwa kupitishwa kwa azimio hilo ni kiashria cha hofu kubwa inayokabili jamii ya kimataifa juu ya hali inayoendelea Ukraine na linatoa msisitizo wa sitisho la mapigano haraka iwezekanavyo, huduma za kibinadamu zifikie walengwa bila vikwazo na mazungumzo na diplomasia vichukue nafasi yake.
Ametua mkutano huo na waandishi wa habari kusema “naungana na nchi nyingine wanachama kuelezea wasiwasi wangu kuhusu ripoti za mashambulizi dhidi ya raia kwenye makazi yao, shule na hospitali, halikadhalika vifo na majeruhi miongoni mwa raia wakiwemo wanawake, watoto, wazee na watu wenye ulemavu.”
Bwana Shahid amesema kama ilivyopendekezwa na wanachama kwenye azimio hilo, anasubiria kwa hamu kupokea ndani ya siku 30 ripoti ya mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu kuhusu hali ya kibinadamu Ukraine, na ameahirisha kikao cha dharura cha 11 cha Baraza Kuu na zaidi ya yote yuko tayari kukiitisha tena pindi itakapotakiwa hivyo na nchi wanachama.
Maoni
Chapisha Maoni