Fahamu mambo sita usiyoyajua kuhusu Sadio Mane wa Senegal na Liverpool
Sadio Mane anayevalia jezi nambari 10 , ametimiza ndoto yake ya kihistoria ya kuisaidia timu yake ya taifa Senegal kushinda kwa mara ya kwanza taji la Afrika.
Mshambuliaji huyo wa Liverpool pia ni maarufu na mzungumzaji. Yeye ni tofauti na wachezaji wengine kama yeye ambao hununua vitu ghali kama vile simu za bei ghali na vitu vinginevyo.
Ni mchezaji anayetoka katika familia masikini ambayo ilikabiliwa na changamoto chungu nzima maishani akiwa mtoto mdogo.
Katika taarifa hii tunakuelezea kuhusu mambo sita kuhusu mchezaji huyu ambaye amepokea uungwaji mkono wa kiwango cha juu mbali na mchezo wake .
1.Alitoroka nyumbani kwao ili kucheza soka
Huenda una ufahamu kuhusu habari hii . Akiwa mtoto mdogo , Mane alikulia katika kijiji kwa jina Bambali nchini Senegal. Wakati huo familia yake haikumruhusu kucheza mpira.
Babake alifariki akiwa na umri wa miaka saba , na alilelewa na wajomba zake. Anatoka katika familia ya Maimamu wa kiislamu. Hivyobasi kitu cha kwanza ambacho mtoto anatarajiwa kupatia kipau mbele ni elimu.
''Baba yangu hakutaka nicheze mpira kwasababu aliamini kwamba elimu ni muhimu kushinda mpira. Ilikuwa vigumu kucheza soka kwasababu yeye hakutaka hivyo'', alisema Mane kwa makala ya BBC.
Mane alielezea kwamba alifurahia sana kucheza soka na hata akalazimika kutumia matunda na mawe akiwa mtoto kwasababu hakuwa na uwezo kupata mpira wakati huo.
Katika kijiji chake ambapo alikuwa maarufu alipatiwa jina la utani la 'BallonBuwa'.
Mwaka 2008 , akiwa na umri wa miaka 16, Mane aliitoroka familia yake na kuelekea mji mkuu wa Dakar ili kutafuta timu.
Alipatikana na kurudishwa nyumbani , na akaahidiwa kwamba hatopelekwa shule mwaka uliofuta na kwamba atapatiwa fursa ya kuendelea kusakata soka.
2. Kazi ya jamii ya kiislamu
Mane anasemekana kutumia fedha nyingi kuwasaidia masikini katika maeneo mengi ya taifa la Senegal. Alitumia fedha zake kusaidia Watoto wadogo mbali na kuwajengea nyumba na vyoo watu masikini. Mapema kanda ya video ilizua hisia huku wengi wakimsifu.
Mwisho wa Twitter ujumbe, 1
3. Alikuwa akimuigiza El Hadji Diouf
Sadio Mane alikuwa na umri wa miaka 10 wakati Senegal ilipotinga robo fainali ya kombe la dunia 2002 na fainali za kombe la bara Afrika Afcon.
Wakati huo kikosi cha taifa cha Simba wa Teranga kilishirikisha Aliou Cisse, Khalilou Fadiga na El Hadji Diouf.
"Wakati huo Senegal ilikuwa na wachezaji bora zaidi'' , alisema Mane
Rafiki yake wa utotoni, Luc, alisema Sadio alikuwa na mifano miwili ya kuigwa: "Wakati huo Sadio alikuwa anavutiwa na Ronaldinho, lakini pia alimpenda El Hadji Diouf, ambaye alitutia moyo sana kucheza soka."
Luc aliongeza kuwa Mane alisema: "Siku moja tutafikia kiwango chao."
Baadhi ya watu sasa wanabishana kwamba Mane sasa yuko juu zaidi ya Diouf - kwani amepata mafanikio zaidi akiwa na Liverpool na kushinda Kombe la Mataifa ya Afrika akiwa na taifa lake.
Kwa hakika, ameifanya Liverpool kuwa na mchezo bora ikilinganishwa na wakati wa El Hadji, ambaye aliichezea klabu hiyo lakini katika miaka ya hivi karibuni amekuwa na mzozo nayo.
4. Ujumbe wa Mane kwa Mohamed Saleh na Nabi Kita
Katika siku za ufunguzi wa Kombe la Mataifa ya Afrika, Mane alirekodi ujumbe wa video kwa wachezaji wenzake wawili wa Liverpool, Mohamed Salah wa Misri na Nabi Keita, mzaliwa wa Guinea.
Akizungumza na wachezaji wote wawili, alisema: "Nina ujumbe maalum kwa marafiki zangu wawili, Nabi Keita na Mo Salah. Kwa bahati mbaya, katika fainali, hakuna timu mbili zinazoweza kukutana, hivyo ni lazima kucheza dhidi ya timu moja. "Najua hilo. itakuwa Misri au Guinea, lakini najua nitawashinda mmoja baada ya mwingine."
Ajabu ni kwamba maneno ya Mane yalitimia na timu nyingine zote barani Afrika zilitolewa kabla hazijatinga fainali, na hatimaye moja kati ya timu mbili alizozitaja ni miongoni mwa timu zilizoingia fainali, Misri.
Mwishoni mwa mechi ya jana usiku, Mane alionekana akimtania Salah ambaye alikuwa amekasirika sana.
5. Mzozo wa hali ya tabia nchi Ulaya
Mnamo 2011, Mane aliondoka Senegal na kujiunga na klabu ya Ufaransa ya FC Metz. Kitu cha kwanza alichogundua alipokwenda Ulaya ni baridi.
Mane anazungumzia kilichompata yeye na wachezaji wenzake alipotoka kwenye vyumba vya kubadilishia nguo akiwa amevalia shati pekee. Alijua hali ya hewa ya Afrika mara nyingi ilikuwa ya joto.
"Wote walianza kunicheka na sikuelewa," alisema. "Waliniuliza, 'Unathubutuje kuvaa nguo hizo?'
6. Shinikizo kutoka kwa mashabiki wa timu ya taifa
Kwa muda mrefu, Mane amekuwa akionesha kiwango kizuri katika soka na klabu alizochezea zimenufaika na kazi yake, lakini amefanya machache kwa nchi yake.
Kwa hiyo, licha ya kupendwa na mashabiki wa nchi yake, walikuwa wakimshinikiza kuikuza Senegal.
Mnamo 2017, hakufanya vyema kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika alipokuwa akiichezea nchi yake. Alishindwa kufunga penalti ili kufuzu katika robo fainali.
Mnamo 2019, hali ilizidi kuwa mbaya baada ya Senegal kupoteza fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Algeria 1-0.
Lakini ni wazi, Mane sasa amepunguza shinikizo kwa timu ya taifa, na katika maeneo mengi ya Senegal ushindi wa timu ya taifa uliadhimishwa kila mahali jana usiku. Mane alifunga bao la mwisho la ushindi dhidi ya Misri.
Maoni
Chapisha Maoni