Baraza Kuu la UN lataka Urusi iondoke Ukraine bila masharti yoyote
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo katika kikao chake maalum cha dharura limepitisha azimio ambalo pamoja na mambo mengine linasisitiza azma yake ya kutambua mamlaka ya Ukraine, uhuru, umoja na mipaka yake ya majini na ardhini inayotambulika kimataifa.
Azimio hilo namba A/ES -11/L.1 limepitishwa kwenye kikao hicho cha 11 cha dharura wakati huu ambapo Urusi inaendelea kushambulia Ukraine ambapo misingi ya azimio hilo pamoja na mambo mengine ni tangazo la tarehe 24 mwezi uliopita wa Februari la Rais Vladmir Putin wa Urusi la kuanzisha operesheni maalum ya kijeshi nchini Ukraine.
Kikao hiki cha dharura kimeitishwa na Baraza la Usalama, ikiwa ni miaka 40 tangu kikao kama hicho kiitishwe kwa lengo la kulinda amani na usalama duniani.
Wajumbe 141 wamepiga kura ya ndio huku 5 wakipiga kura ya hapana na wengine 35 hawakupiga kura yoyote, ambapo kwa mujibu wa kanuni za Baraza Kuu katika kikao kama cha leo kura zinazohitajika kupitisha azimio ni theluthi mbili za wajumbe walioko kwenye kikao.
Vipengele muhimu kwenye azimio
Azimio linalaani vikali uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine ikiwa ni kinyume na kipengele namba 4 cha Ibara ya 2 ya Chata ya Umoja wa Mataifa.
Azimio pia linataka Urusi isitishe mara moja matumizi ya nguvu za kijeshi dhidi ya Ukraine na ijizuie dhidi ya vitisho vyovyote kinyume cha sheria au matumizi ya nguvu za kijeshi dhidi ya mwanachama yeyote wa Umoja wa Mataifa.
Urusi pia inatakiwa iondoe mara moja na bila masharti yoyote vikosi vyake kutoka eneo la mipaka ya Ukraine inayotambulika kimataifa.
Azimio linataka pia Urusi ibadili kauli yake kuhusu hadhi ya baadhi ya maeneo ya Donetsk na Luhansk huko Ukraine.
Kuhusu misaada ya kibinadamu, azimio linataka pande zote kwenye mzozo huo kuruhusu ufikishaji wa misaada bila vikwazo vyovyote kwa wahitaji nchini Ukraine sambamba na kulinda raia wakiwemo wafanyakazi wanaotoka misaada ya kibinadamu na watu walio hatarini kama vile wenye ulemavu, wanawake, watoto wazee, wahamiaji, na watu wa jamii ya asili.
Kwa upande wake, Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa misaada ya kibinadamu ametakiwa katika siku 30 kuanzia leo awasilishe kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hali ya kibinadamu nchini Ukraine na hatua za kibinadamu zilizochukuliwa.
Azimio limekaribisha hatua za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, nchi wanachama na mashirika ya kikanda za kusongesha harakati za kusaka suluhu na kutaka hatua zaidi.
Michango ya wajumbe
Kwa kiasi kikubwa wajumbe walikuwa na maoni ya kuitaka Urusi iondoe vikosi vyake nchini Ukraine kwa mujibu wa Chata ya Umoja wa Mataifa inayopinga uvamizi wa taifa moja dhidi ya lingine. Marekani ilipigia chepuo upigiaji wa kura ya Ndio kwa azimio la leo ambapo Mwakilishi wake wa kudumu kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Linda Thomas-Greenfield alisema “piga kura ya ndio iwapo unaamini kuwa taifa lako lina haki ya mamlaka ya mipaka yake na uhuru.”
Hata hivyo Mwakilishi wa kudumu wa Belarus kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Valentin Rybakov alisema “tunapiga kura ya hapana dhidi ya azimio hili kwa sababu tunaamini azimio hili lilipaswa kuwa na kipengele kimoja tu cha kuepusha chuki na si vinginevyo.” Amedai kuwa Belarus kwa upande wake inaratibu mazungumzo kati ya Ukraine na Urusi lakini cha ajabu hakuna nchi inayotilia maanani.
Rwanda kwa upande wake imesema imeunga mkono azimio hilo kwa kutambua kuwa inaunga mkono Chata ya Umoja wa Mataifa huku ikisema Urusi na Ukraine ndio zenye ufunguo wa kumaliza mgogoro unaoendelea huku ikisema harakati zozote za muingilio wa kigeni kwenye mzozo huo utafanya hali kuwa mbaya zaidi.
India kwa upande wake ikaeleeza masikitiko yake juu ya ghasia hasa kwa wanafunzi wakiwemo wale wa India. Mwakilishi wa India kwenye Umoja wa Mataifa Balozi T. S Tirumurti ametaja tukio la kuuawa kwa raia wa India hapo jana kwenye mji wa Kharkiv huku akishukuru nchi jirani na Ukraine ambazo zimefungua mipaka yao kuruhusu raia wa nchi ya tatu kuingia. Amesema tayari India imetuma ndege kuchukua wanafunzi wake walioko Ukraine na kusisitiza kuwa India ambayo haikupiga kura kuonesha msimamo wowote inaamini tofauti zozote zinaweza kumalizwa kwa mazungumzo.
Nchi zilizoepuka kupiga kura
Miongoni mwa nchi 35 ambazo hazikupiga kura kuonesha msimamo wowote ni Tanzania, Uganda, India, Bolivia, Burundi, Namibia, Msumbiji na Equatorial Guinea.
Msingi wa vikao vya dharura vya Baraza Kuu la UN
Kikao cha dharura cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ni kikao ambacho kwa kawaida hakiko kwenye ratiba ya Baraza Kuu na huitishwa kwa ajili ya suala mahsusi. Kupitia Sura ya 5 ya Chata ya Umoja wa Mataifa, Baraza la Usalama kwa kawaida ndio lenye wajibu wa kusimamia masuala ya amani na usalama duniani.
Hata hivyo tarehe 3 mwezi Novemba mwaka 1950, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio namba 377 ambalo lilipanua wigo wa mamlaka ya kuzingatia mada ambazo awali zilijikita kwa Baraza la Usalama pekee. Kupitia azimio hilo, iwapo Baraza la Usalama linashindwa kufikia kauli moja juu ya suala fulani, Baraza Kuu linaweza kuitisha kikao cha dharura ndani ya saa 24 kujadili suala hilo.
Maoni
Chapisha Maoni