Askofu Ruwa'ichi awataka wakatoliki kuiombea Ukraine
WEDNESDAY MARCH 02 2022
Dar es Salaam. Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Mhashimu Yuda Thadeus Ruwa'ichi, amewataka wakristo wakatoliki nchini wanapoingia katika kipindi cha kwaresma kuungana kwa pamoja kuiomba nchi ya Ukraine ambayo kwa sasa ipo katika misukosuko ya vita na Russia.
Askofu Ruwa'ichi ameyasema hayo leo Machi 2, 2022 jijini Dar es Salaam wakati wa mahubiri yake aliyoitoa kwenye adhimisho la Misa Takatifu ya Jumatano ya majivu katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Posta.
Ruwa'ichi amesema wanapaswa kuungana na Ukraine kama ambavyo wamekuwa wakiomba msaada kwa mataifa mbalimbali ili kukomesha vita hiyo.
"Tuzame katika sala tukimuomba Mungu awarudishie amani yao nchi ya Ukraine na waweze kuingia kwenye makubaliano ya amani na Russia, lakini tusiishie kuiombea tu Ukraine bali na mataifa mengine pia ambayo yapo katika vita ili wawe tayari kuwa na makubaliano ya amani hatimaye wamtukuze Mungu," amesema .
Amesisitiza kuwa wanadamu wasiwatazame wayahudi kama wale watu waliomsaliti kristo bali watambue kuwa kadri wanavyozidi kutenda dhambi nao wanamsaliti kristo na kuendelea kumuumiza.
Hata hivyo amesema kipindi cha kwaresma wanakanisa wanapewa fursa ya kutenda matendo mema huku wakidokeza maneno ya Mungu kufanya toba halisi na sio ya kinafki
"Neno la Mungu linatualika na kutuelekeza jinsi ya kuishi katika toba hii, ameanza kwa kutufundisha namna ya kuenenda ndani ya mioyo yetu ili tupate uongofu, tumrudie Mungu na tuanze upya.
"Tuwe makini tusiingie kwenye kishashiwi kwa kuzama kwenye toba ya matendo ya nje nje, yaani toba isiyogusa mioyo wala undani wetu na ndio maana tunaambiwa turarue mioyo wala siyo mavazi yetu. Sisi ni taifa jipya la Mungu na anasema tuzame na tumrudie kwa dhati Mungu wetu katika kipindi hiki cha Kwaresma," amesema
Maoni
Chapisha Maoni