MADALALI wa Kariakoo Auction Mart wametifuana na uongozi wao wakiwatuhumu viongozi hao kukaa madarakani kwa zaidi miaka saba bila kufanyika uchaguzi wa kupata viongozi wapya wakati katiba yao inasema uongozi unatakiwa kukaa madarakani miaka mitatu na kufanyika uchaguzi.
Madalali hao wamesema kilio chao kikubwa kwa uongozi huo licha ya kukaa madarakani muda mrefu wamekuwa hawana maendeleo kwenye umoja wao huo.
Wakiendelea kuwatuhumu viongozi wao madalali hao wamewaomba viongozi mbalimbali wa serikali kufika kwenye ofisi yao na kuangalia mazingira wanayofanyia kazi ili wajionee wenyewe.
Hata hivyo wanahabari wetu waliutafuta uongozi wa madalali hao na kufanikiwa kuzungumza na Katibu wao aliyejitambulisha kwa jina la Swalehe Omari Msoka ambaye alikiri uongozi wao kukaa madarakani kwa zaidi ya miaka saba kinyume na katiba yao lakini akafafanua kuwa hilo limesababishwa na migogoro ya mara kwa mara ya madalali hao inayosababisha uchaguzi kuahirishwa kila unapopangwa kufanyika.
Katibu huyo aliendelea kufafanua;
“Ni kweli katiba yetu inasema tufanye uchaguzi kila baada ya miaka mitatu lakini tatizo limekuwa hawa jamaa kila unapokaribia uchaguzi waanzisha vurugu na uchaguzi unaahirishwa ndiyo maana mpaka leo bado hawajapatikana viongozi wapya kama wanavyotaka.
“Wamekuwa wakiutuhumu uongozi kutofanya maendeleo ya hili eneo, hilo nalo linasababishwa na migogoro hiyo ambapo tumeshampata mwekezaji lakini naye wamekuwa wakimkataa hivyo hawezi kuanza kufanya maendeleo kabla hali haijawa shwari.
“Wamekimbilia mahakamani kutushitaki viongozi lakini hata huko pia wataambiwa wafuate utaratibu na sio kama wanavyotaka wao.” Alimaliza kusema Katibu huyo.
Kesi hiyo inatarajiwa kusikilizwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam Machi 8 mwaka huu ambapo huenda ikatolewa uamuzi.
Maoni
Chapisha Maoni