Fahamu umuhimu wa ziara ya Rais Samia Ulaya kwa Watanzania
- Beatrice Kimaro
- Mchambuzi, Tanzania
"Tanzania itakuwa sawa na Ulaya ndani ya miaka 6", hii ilikuwa kauli ya Rais wa taifa hilo, Samia Suluhu Hassan mara baada ya kurejea nyumbani mwishoni mwa wiki akitokea barani Ulaya alikokuwa na ziara ya kikazi katika nchi za Ufaransa na Ubelgiji.
Ni kauli iliyoibua mjadala mkubwa. Wapo wanaojiuliza itawezekanaje? Na wapo wanaoona inawezekana. Lakini hilo halizuii mtazamo wa namna ziara hiyo ilivyoleta sura tofauti kwenye nyanja ya kidiplomasia na fedha za maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa taifa hilo la Afrika Mashariki.
Siku 10 za ziara hiyo zimefungua milango ya mahusiano ya kidiplomasia, kiuchumi na kijami, milango ambayo ilifungwa kwa 'kufuli la chuma' katika kipindi cha utawala wa awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli.
'Kipindi kile ambacho hatukuwa vizuri walifikia hatua ya kuzuia fedha za miradi ambayo Tanzania iliomba lakini sasa wamefungua kila kitu kiko vizuri", anasema Rais Samia kwenye moja ya mahojiano yake kuhusu ziara hii.
Hasara za kufunga mlango wa mahusiano hasa na nchi za Umoja wa Ulaya zilikuwa kubwa zaidi kuliko faida. Lakini ziara hii ina maana yoyote kwa mtanzania? Jibu fupi na rahisi ni ndiyo, kwa sababu nyingi tu lakini hizi ni miongoni mwao;
Fedha za Miradi
Kwa mujibu wa Rais Samia, amefanikiwa kupata fedha za msaada kiasi cha Euro milioni 450 sawa na Shilingi trilioni1.17 kutoka Umoja wa Ulaya (EU) ikiwa ni sehemu ya Euro bilioni 55 zilizotengwa na Umoja huo kwa ajili ya Afrika kukabiliana na janga la Covid 19.
Katika kipindi cha cha miaka mitatu ijayo fedha hizo zitatumika kukwamua miradi iliyokwama ya viwanja vya ndege Kigoma, Shinyanga na Pemba, ukarabati wa uwanja wa ndege wa Julius Nyerere Dar es Salaam (Terminal II), Mafunzo, mradi wa mabasi ya umeme, ukamilishaji wa mradi wa mabasi ya mwendo wa haraka na kilimo.
Euro milioni 450 ni fedha zinazoweza kuchochea maendeleo ya nchi kwa kasi. Uwepo wa fedha hizi mbali na malengo yake ya moja kwa moja, utaongeza pia mzunguko wa fedha mtaani na kuchangamsha shughuli za uchumi kwa wananchi. Shughuli za uchumi zikichangamka, unatengeneza ajira na kuongeza kipato cha watu, mwishowe unaboresha maisha yao kwa sababu wataweza kumudu kununua bidhaa, huduma na mahitaji muhimu kuendesha maisha yao.
Mwishoni mwa mwaka jana Tanzania ilipokea mkopo wa shilingi trilioni 1.3 uliotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF), kwa ajili ya kushughulikia janga la Corona. Mkopo huu umesaidia ujenzi wa maelfu ya madarasa nchi nzima na kutafsiri vyema mpango wa serikali ya Tanzania wa kuinua uchumi wake na wa watu wake. Kama zilivyo kwa fedha hizi, fedha za 'Ulaya' alizozipata Rais Samia kama zitatumika vyema, zitasaidia kuinua sekta lengwa.
'Ziara ya Samia, bila shaka ina faida kubwa, lakini kupata fedha hizi ni jambo moja, japo la pili na la muhimu, lazima fedha hizi zisimamiwe vyema ili zipelekwe kwenye lengo husika lenye faida kwa wananchi', alisema Profesa Balthazari Namwata wa Chuo kikuu cha Ushirika Moshi.
Kusafisha uhusiano wa kiplomasia
Katika kipindi cha miaka sita iliyopita Tanzania ilisakamwa kwa kutokuwa na mahusiano mazuri kidiplomasia na Jumuia ama nchi zingine. Rais wa wakati huo, Magufuli, alipendelea kutuma wawakilishi katika mikutano mingi mikubwa na hakuwahi kusafiri kwa ziara yoyote ya kikazi nje ya bara la Afrika.
Hata kwa ziara zake ndani ya Afrika, alizuru nchi tisa tu kati ya nchi zaidi ya 50 katika wakati wote huo, akitembelea nchi za Rwanda, Kenya, Ethiopia, Burundi, Uganda, Afrika Kusini, Namibia, Malawi na Zimbabwe.
Lakini katika kipindi cha chini ya mwaka mmoja Rais Samia ameshatoka kwa uwiano mara nyingi zaidi ya mtangulizi wake. Na safari hii akienda Ulaya ambapo uhusiano wa Jumuia ya bara hilo na Tanzania umedumu kwa miongo zaidi ya mitani.
Rais Samia mwenyewe anakiri kwamba katika kipindi hicho uhusiano wa Tanzania na Jumuia ya Ulaya ulikuwa na changamoto.
"Wakati ule ulikuwa ni mtazamo, tulikuwa tunaangalia mambo ya EPA (Mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi), kulikuwa kuna kugongana gongana kwenye ideology kwenye siasa, labda Ulaya walisema jambo ambalo halikutupendeza, lakini baada ya muda tumezungumza na yote yako sawa sasa", anasema Rais Samia.
Maoni
Chapisha Maoni